Sehemu ya kwanza

Wakati ana umri wa miaka hamsini na tano, Majaliwa alikuwa bado anafanya kazi ya ukuli. Kazi hii aliianza wakati yungali kijana wa miaka ishirini na moja. Mazoea ya kazi hiyo yalimfany a aimudu vizuri kabisa. Alikuwa mtu mashuhuri sana miongoni mwa wafanyakazi wa bandarini. Dongo la Majaliwa lilikuwa zuri sana kwani hata katika umri wa miaka hamsini na tano alionyesha kama kijana wa m iaka thelathini tu. Alikuwa na urefu wa wastani na mwingi wa mwili.

Majaliwa ailikuwa mwingi wa heshima, lakini pindi alipokuwa kazini, aliziweka heshima hizo pembeni na kushika masihara na matusi kama ilivyo tabia ya mkuli. Lakini palipotokea matatizo alikuwa ni mtu wa busara na mwingi wa huruma. Mara kwa mara aliwanasihi wenzake waliokabiliwa, na matatizo namna kwa namna hata ikawa kila walipokuwa na matatizo ya kinyumbani, wafanyakazi wengi wa bandarini, walimhadithia Majaliwa ili awape nasaha na maongozi.

Majaliwa alikuwa na mkewe aliyeitwa Mashavu. Ijapokuwa Majaliwa na Bi Mashavu walioana walipokuwa vijana, kwa muda mrefu walikuwa hawakubahatika kupata mtoto. Walikata tamaa ya kupata mtoto na hakuna mzimu walioubakisha tokea Unguja hadi Pemba katika jitihada za kuomba mtoto. Walipata mtoto wao wa kwanza na wa mwisho wakati wote wawili wameshakuwa watu wazima. Siku aliyozaliwa mtoto huyo, furaha ya wazee wawili hao ilikuwa haina kifani. Alikuwa mtoto mwanamume, wakampa jina la Rashidi .

Tokea kuzaliwa Rashidi, baba yake aliendelea kufanya kazi yake iliyompatia maisha na kumlea Rashidi. Alikuwa hodari wa kuamka alfajiri; ila siku moja mpaka saa moja na nusu alikuwa bado amelala, amejifunika shuka gubigubi.

Mashavu alikuwa jikoni, na kwa ajabu aliyoiona kwamba mumewe bado hajaamka mpaka saa zile, ilimfanya arejee chumbani kumsikiliza mume wake. Alikuja mbele ya mlango wa chumba chao na kusimama mbele. Alimtazama mumewe na alipoona hana dalili ya kuamka alimwuliza :

Fanya Mazoezi ya Sehemu ya Kwanza.

Sehemu ya pili

"Leo huendi kazini? "

"Siendi," alijibu Majaliwa huku akiwa bado yupo kitandani.

"Kwa nini?"

"Ah! Wacha kunikera na mchukue huyo mtoto awache kupiga makelele.

Rashidi, ambae alikuwa bado mchanga, alikuwa amekwisha kuamka, akawa analia kwa kelele kubwa.

Bi Mashavu alimbeba Rashidi ambaye mara alinyamaza kulia, na hapo Bi Mashavu alianza kumwuliza tena Majaliwa: "Sasa bwana leo kwa nini hutaki kwenda kazini?"

"Si kama sitaki kwenda kazini, nataka sana; lakini leo najahisi hali yangu naumwa umwa, nahisi kama homa na kizunguzungu."

"Sasa si bora nikakutelekea maji ya moto ujimwagie labda utapata nafuu?"

"Haya," Majaliwa alijibu.

Bi Mashavu alimfunga Rashidi katika ubeleko na hapo hapo alirejea jikoni na kuteleka maji ya moto. Vile vile alipika uji wa mapande na kuujaza pilipili manga kwa matu-maini kwamba huenda ukamsaidia mumewe kupata nafuu.

Majaliwa alikuwa hapendi kulala bila ya kwenda kazini kwa kuhofia mambo nyumbani yangekwenda mrama. Shillingi mbili ambazo alizipata kwa kutwa zilitumika kwa matumzi ya nyumbani isibaki hata senti moja. Na wala si kama pesa hizo zilitosha, bali ilimlazimu azifanye zitoshe.

Maji ya moto yalipokuwa tayari, Majaliwa aliingia chooni na kukoga na baada ya kumaliza alikunywa bakuli moja la uji wa mapande na kurejea kitandani.

"Sasa leo bwana nini shauri ?" Bi Mashavu aliuliza kutaka kujua habari ya chakula cha siku ile ambayo mumewe hakwenda kazini.

"Nitajikongojea hivyo hivyo mpaka hapo kwa Hajitumbo nikatafute cho chote," Majaliwa alijibu huko yupo kitandani amejifunika shuka gubigubi.

Ilipofika saa nne, Majaliwa ilimbidi kutoka na hakusimama mpaka kwa Hajitumbo. Haikuwa masafa marefu kutoka Mferejimaringo mpaka hapo na baada ya kufika tu alinunua fungu la muhogo na papa mkavu na hiyo ilitosha kwa chakula cha siku ile. Ama kwa Rashidi, unga wa mtaa ulikuwepo nyumbani na hicho ndicho kilichokuwa chakula chake cha siku ile.

Fanya Mazoezi ya Sehemu ya Pili.

Sehemu ya Tatu

Siku ya pili Majaliwa alijihisi mzima na kama kawaida yake alfajiri aliamka. Alivalia magwanda yake na kwenda zake gatini ambako kazi ngumu ilikuwa ikimngojea.

Siku ile kulikuwa na kazi ya kuteremsha vyuma vya njia ya reli iliyokuwa ikijengwa huko Tanganyika. Vyuma hivyo viliteremshwa Unguja ili baadaye visafirishwe tena mpaka huko Dar es Salaam.

Aliopoingia tu gatini, Majaliwa alikutana na Akida na bila ya kusalimiana Akida alianza masihara, "Jana hatukukuona jee, mama etu alikzuia nini ?"

"Nilipigwa na homa ya ghafla," Majaliwa alijibu.

"Ah, twambie kweli bwana," Akida alizidi kuendelea na masihara yake.

"Unataka nikwambie kweli?" Majaliwa nae alianza masihara. "Nikikwambia kweli halafu utakasirika, kwani hujui kama mimi ni shemaji yako na yeye nd'o alienizuia nisije kazini jana?"

"Ha, ha, ha," Akida alicheka kwa kelele na kusema, "Ama mzee weye unpenda kujigamba."

Majaliwa na Akida walikuwa wamefuatana pamoja kwani wote walikuwa katika kikundi kimoja.

Meli ilikuwa imeshafunga gati, waendeshaji kreni wameshapanda juu ya kreni zao, na mara harakati za kuteremsha vyuma zilianza.

"Lete! Lete! Lete!" Shaabani, mkuu wa kikundi cha akina Majaliwa alikuwa anamwongoza mwendeshaji wa kreni wakati vyuma vinateremshwa.

Makuli walikaa kwa hadhari hapo chini wakkifungua chuma kimoja baada ya kuteremshwa.

Kila baada ya kuteremshwa, chuma hicho kilichukuliwa na watu wanne na kupelekwa mpaka nje ya uwanja wa gati ambako vyuma hivyo vilipangwa.

Kazi hiyo ngumu ilimalizika kazi tu, Majaliwa hakusimama mpaka kwake. Alipofika nyumbani alimkuta Rashidi kachafuka, kelele nyumba nzima, analia huku Bi Mashavu amempakata anachochea mmoto jikoni huku akimbembeleza:

Fanya Mazoezi ya Sehemu ya Tatu.

Sehemu ya Nne

"Nini tena unamwacha mtoto analia tokea saa ile?" Majaliwa ambae alikuwa chumbani akivua nguo aliuliza kwa hamaki.

"Ah, hata sijui kinachomliza mtoto huyu," Bi Mashavu alisema.

"Mynyonyeshe basi, labda ana njaa," Majaliwa aliamrisha.

"Ntamnyonyesha vipi nami n'na chungu jikoni?" Bi Mashavu alijibu akiwa naye kisha hamaki.

Joto pamoja na moto wa jikoni ndiyo yaliyokuwa yamkimliza Rashidi. Bi Mashavu hakuwa na wa kumsaidia, alikuwa peke yake ndani ya nyumba; msaidizi wake alikuwa mumewe Majaliwa.

"Njoo umchukue basi utoke nae nje labda atanyamaza ," alisema Bi Mashavu.

Majaliwa alivua nguo zake za kazini na kuzitundika juu ya kamba chooni, alijifunga shuka yake kiunoni na hapo tena alimchukua Rashidi na kutoka naye nje.

Majaliwa alikuwa akimpenda mwanawe, kwani huyo alikuwa ni mwana mjukuu. Alitoka naye nje na kukaa barazani na baada ya kucheza naye kwa muda mfupi Rashidi alilala. Hapo tena Majaliwa alipata nafasi ya kwenda kugoga na kupumzika kidogo.

Majaliwa aliingia chumbani huku akimwacha Bi Mashavu akipakua chakula.

Ijapokuwa chumba hicho kilikuwa kidogo, Bi Mashavu alikiweka katika hali ya usafi kabisa. Kitanda cha samadari kilichokwemo humo kilitandikwa vizuri kwa shuka nyeupe iliyofumwa maua mekundu katikati. Mlikuwa na viti viwili vya 'murscheya' vilivyokuwa na mito ya usumba ambayo ilivishwa foronya safi nyeupe. Kila magharibi Bi Mashavu alikuwa na kawaida ya kunyunyiza asumini juu ya kitanda na baadaye kufukiza udi ambao ulileta harufu nzuri ndani ya chumba hicho. Kila siku kanga safi zilining'inizwa juu ya besera ya kitanda na Majaliwa, baada ya kwisha kukoga tu, alivuta moja ya kanga hizo na kujifunga kiunoni.

"Bwana, chakula tayari," Bi Mashavu alimwambia Majaliwa, aliyekuwa amejinyosha juu ya kitanda kile kilichotandikwa vizuri huku amemlaza Rashidi uvauni pake.

Bi Mashavu naye alikuwa amekwisha koga, amejifunga kanga moja kifuani na moja amejitanda. Amejitia tarabizuna ananukia vizuri. Sinia ya chakula iliwekwa katikati ya chumba na hapo tena Majaliwa na Bi Mashavu walikaa juu ya mkeka na kuanza kula.

Huo ndiyo uliokuwa wakati wao wa starehe. Bi Mashavu amempakata Rashidi, Majailwa amejifunga kanga moja tu tumbo wazi.

"Rashidi kawa mtundu siku hizi," Bi Mashavu alianza mazungumzo, "leo nilimuacha hapo katikati kidogo tu mara namsikia yupo nje, tokea amejua huko kutambaa imekuwa shida."

Nd'o mwanarnume, lazima awe mtundu ," Majaliwa alisema.

" Unajionaje hali yako leo, ile homa imepungua?" Bi Mashavu aliuliza.

"Leo sijambo khassa ," Majaliwa alijibu.

Majaliwa alikuwa si mtembezi wa usiku, hatoki isipokuwa ana haja muhimu kwa hivyo walipomaliza ula tu alitoka nje kupunga upepo na hii ndiyo iliyokuwa kawaida yake kila siku.

Fanya Mazoezi ya Sehemu ya Nne.

Sehemu ya Tano

Siku ya pili kazi ya kuteremsha vyuma vya njia wa reli iliendelea. Kila chuma kimoja, kama kawaida, kilichukuliwa na watu wanne.

"Chukua vizuri!" Majaliwa ambaye alikuwa nyuma kabisa alimpigia kelele kuli mwenzake aliyeonyesha amelegea kidogo na ambaye alikuwa kati.

Walikibeba chuma hicho mpaka pale uwanjani vinapokusanywa vyuma vyote. Wakati wa kukitua chuma hicho iliwabidi wote wakitue kwa umoja wao.

"Tayari, tayari?," aliuliza yule aliyekuwa nyuma kabisa alimpigia mbele kisha akaamuru, "Haya tupa!"

Wote walikitupa kile chuma lakini kwa bahati mbaya yule aliyekuwa kati alichelewa kidogo na uzito wote wa chuma kile ukamwelemea yeye begani na mfupa wa bega lake la kuume ukadata.

"Aaaaa!" akaanguka huku akipigia kelele nyingi kwa maumivu. Wafanyakazi wenzake na wengine waliokuwa karibu walimzunguka huku wakijaribu kumsaidia mfanyakazi mwenzao aliyekuwa akipiga mikambe kama mtu mwenye kukata roho. Pale pale alikwenda kuitwa mkuu wa gati ambae alikuwa Mwingereza. Muda si muda alifikia pale alipo majeruhi yule. Alimbonyeza bonyeza na kumfanya yule mfanyakazi azidi kupiga makelele kwa maumivu na mara yule Mzungu akasema, "Sasa peleka yeye nyumbani."

"Tumpeleke nyumbani?" Akida aliuliza. "Lazima tumpeleke hospitali, ameumia sana huyu," aliendelea.

"Nani tapeleka yeye hospitali?" Yule Mzungu aliuliza.

"Gari ya kampuni si ipo?" Wote waliopo pale walisema kwa umoja wao.

Yule Mzungu ambaye alikuwa amechutama huku akimgeuza geuza majeruhi yule alisimama na kuwatazama wafanyakazi wale mmoja mmoja na kwa ukali alisema, "Nyinyi hapana jua kama gari ya kampuni iko kazi mingi?"

"Muhimu hiyo kazi au huyu mtu aliyeumia? Unafikiri kazi muhimu kuliko maisha ya mtu?" Akida aliuliza kwa hamaki.

"Hiyo hapana shauri yangu," alijibu yule Mzungu na bila ya kumtazama yeyote katika watu wale waliokuwapo pale alikwenda zake.

Makuli wote walipigwa na mshangao, hawakujua la kufanya; mwenzao amelala chini mahtuti, kauli hana, amebakia kuugua tu kwa maumivu makubwa aliyokuwa nayo.

"Mie n'na shauri moja", Majaliwa alisem kwa ghafla, " tuchageni, na pesa zitakazopatikana tutakodi gari tumpeleke hospitali."

Hapana aliyepinga shauri lile na hapo hapo upatu wa maridadi ulianza. Aliyekuwa na senti ishirini, aliyekuwa na senti hamsini, almuradi kila mtu alitoa alichokuwa nacho. Kwa jumla zilipatikana shilingi kumi na hapo hapo mmoja alitoka kwenda kukodi gari na baada ya kupatikana gari hiyo majeruhi yule alipelekwa hospitali.

Makuli wote waliona unyonge mkubwa kwa ajali iliyompata mwenzao siku ile na walikuwa na hakika kwamba asingeiweza tena kazi ya ukuli.

Majaliwa alirejea nyumbani na huzuni kubwa. Fikira zake zote zilikuwa kwa yule mfanyakazi mwenzake ambaye maisha yake yalikwisha potea kwa kazi ya shilingi mbili.

Fanya Mazoezi ya Sehemu ya Tano.

Sehemu ya sita

Alipofika nyumbani hakusema na mtu ila aliingia chumbani na kukaa juu ya kiti bila ya hata kuvua maguo yake machafu ya kazini. Alikaa pale na kujikamata kichwa.

Bi Mashavu alipigwa na mshangao kwani hii ilikuwa siyo kawaida ya mumewe. Hakustahimili kule jikoni alikokuwapo akipika, alimfuatia mumewe chumbani ambako alimkuta alijiinamia kichwa chake amekizamisha ndani ya viganja vyake viwili vya mikono. Akamwuliza "Mbona hivyo leo bwana, ile homa imekurejea nini?"

"Sina homa, " Majaliwa aiijibu kwa sauti ya chini.

"Sasa cha mno nini tena?"

"Ah, mwenzetu mmoja ameumia sana leo kazini na sijui hali yake namna gani hivi sasa."

Bi Mashavu hakutaka kuendelea na mazungurnzo hayo kwani alihisi akitaka kuyajua zaidi atamzidishia unyonge mumewe. Aliusindika mlango wa chumba na taratibu alirejea jikoni na Rashidi wake mgongoni.

Hii haikuwa ajali ya kwanza bandarini hapo, ajali nyingi kama hizo na mbaya zaidi zilitokea. Katika ajali nyingine wafanyakazi walipoteza maisha yao na wengine walibakia viwete maisha yao; wengi katika wao wakiishia kazi ya kuomba. Wafanyakazi wa bandarini hawakuweza kufanya lolote ila kulalamika tu.

Siku nenda siku rudi Majaliwa aliendelea kufanya kazi ya ukuli. Kila alipoendelea kukonga afya ilizidi kumpungua, lakini hata hivyo ilirnlazimu kuendelea na kazi ili aweze kuendesha maisha yake yeye, mkewe na mtoto wake.

Majaliwa aliendelea na kazi ya ukuli mpaka ikamvunja kabisa na hatimae alipatwa na ugoniwa wa kiarusi ambao ulimlaza kitandani mpaka kufa kwake. Alifia hapo hapo Mferejimaringo na makuli wengi walihudhuria maziko yake hapo Makaburimsafa.

Baada ya kifo cha Majaliwa, Bi Mashavu ilimbidi afanye kazi ili aweze kuendesha maisha yeye na mtoto wake Rashidi ambae sasa alikuwa mkubwa. Hakuna kazi aliyoweza kuifanya isipokuwa kazi ya biashara ndogo ndogo kama vile kupika maandazi, kupika mboga na biashara nyingine kama hiyo. Rashidi alimsaidia mama yake katika kazi zake zote; siku nyingine alitembeza mikate ya kusukuma au maandazi na siku nyingine alitembeza mihogo ya kuchemshwa.

Rashidi hakuweza kuishi katika hali hii na baada ya kufikiri sana aliona bora atafute kazi ya kuweza kumsaidia yeye pamoja na marna yake Bi Mashavu. Kazi ya kwanza aliyofikiria ilikuwa ni kazi ya marehemu baba yake, kazi ya ukuli.

Fanya Mazoezi ya Sehemu ya Sita.