Sura ya Pili


King'ora kimelia. Ni saa moja na nusu asubuhi. Watu wamekasirika na mamia yao wameuzonga mlango wa chuma unaowazuia wasiingie ndani ya bandari ya mji wa Unguja.

Kelele, matusi na malalamiko; vijana, watu wazima hata watoto, wote wakiwa wamevaa nguo chafu zilizoraruka, nyingine zikiwa zimepoteza rangi yake ya awali kwa kupauka na kwa kutiwa viraka vya rangi mbali mbali.

Nyama ya mlango wa chuma asimama Mhindi mmoja na vipande vya karatasi vya rangi ya kibuluu, anavigawa lakini kwa wale tu walio na nguvu ya kuvinyakua kutoka mkononi mwake. Kila anapotoa kipande kingine mwitu wa mikono unakigombania. Hapa panatumika mabavu tu, hapana cha huruma wala utu. Lakini pamoja na mabavu hayo pana kujuana vile vile. Anayefahamiana na yule Mhindi mwenye kugawa vile vipande anaweza kukipata kipande kwa urahisi. Mhindi huyo anawaelewa wale wenye nguvu na walio mahodari kwa kazi za kichukuzi. Shida ni kwa wale 'wageni', wale ambao warnefika hapo kwa mara ya kwanza katika vita hivyo vya kutafuta kazi.

Hii ndiyo mandhari Rashidi aliyoikuta bandarini. Hapa ndipo baba yake aliponyonywa uhai wake akafa.bila cho-chote. Unguja bandarini. Mwaka 1948.

"Hapa, hapa, na mie," Rashidi naye alipiga kelele.

Sauti yake ya kitoto haikuweza kusikika katikati ya sauti kadha wa kadha za watu waliokasirika.

Rashidi alikuwa ni kijana mdogo mwenye umri wa miaka kumi na sita tu. Hakupata nafasi ya kusoma skuli kwani tokea kuinukia kwake ilimbidi afanye kazi yoyote ilekumwe-zesha kumsaidia mama yake kuendesha maisha.

Rashidi hakuwa mrefu lakini vile vile hakuwa mfupi sana. Alikuwa na kifua kipana kilichovimba kwa misuli aliyokuwa nayo. Mikono yake iliyoviringana na umbile hili pamoja na sura yake ya kitoto ilimfanya Bwana Ramju, yule Mhindi ali-yekuwa anagawa vipande amtupie macho.

"Wewe naweza kazi?"

Kabla Rashidi hajajibu, Bwana Ramju alivutwa shati na mkono mmoja ulimfikia pale aliposimama nyuma ya lango la chuma. Kuangalia, Bwana Ramju alimkabili mtu mwingine na bila kupoteza wakati alimpa kimoja katika vile vipande vya karatasi vya rangi ya kibuluu alivyokuwa navyo mko-noni. Yule mtu alijisukuma nyuma kwa nguvu akijitoa katika kundi la watu waliokuwa wakiminyana mbele ya lile lango la chuma.

Mwenye bahati yake alipata kazi pale na wasiokuwa na bahati walitawanyika kwenda kutafuta kazi mahali pengine.

"We mtoto unatafuta nini huku?" Ghafla Rashidi aliu-lizwa na mtu aliyempiga kumbo huku akiwa amebeba gunia zito. Bila ya kumtazama Rashidi mara ya pili yule mtu aliendelea na safari yake na gunia lake begani, mbio.

Rashidi, akiwa ni mmoja miongoni mwa waliokosa kazi siku ile alikuwa akizunguka huku na huku taratibu akifikiri nini la kufanya.

Wote wale waliokuwa wakisukumana mbele ya lango la chuma walitawanyika, na kwa wingi wao walizidisha zogo na kelele zilizokuwepe mbele ya jengo lililoizunguka bandari ya Unguja.

Hapo ndipo palipokuwa pakiletwa mali yote ya wakulima wa Unguja na Pemba kuuzwa kwa matajiri ili waisafirishe kwenda nchi za nje.

Milio ya magari yaliyokuja kutoka schemu mbali mbali za mashamba yakiwa yamesheheni bidhaa za karafuu, mbata, pilipili na mazao mengine ilizidisha zaidi ile zogo na kelele katika eneo hilo.

Wachukuzi waliokuwa wakiburura marikwama mbio huku wakinguruma kwa umoja wao waliwahmanisha watu wa hapo na hakuna hata mmoja aliyethubutu kuzubaa.

"We mtoto utakufa wee!" Rashidi alivutwa mkono na mtu asiyemujua na dakika ile ile lilimpitia gari la matwana lilolosheheni magunia ya karafuu juu ya kipaa.

Sehemu hiyo yote ilihanikizwa na kelele za matishari yaliyokuwa yakigongwa. Hewa ya hapo ilinukia harafu nzuri ya karafuu iliyotoka kwenye kiwanda kidogo cha kutengenezea mafuta ya makonyo ya karafuu kilichokuwepo hapo. Lakini mara nyingi hewa hiyo nzuri iliharibiwa na harafu mbaya ya papa, nguru na samaki wengine wakavu waliokuwa wakiteremshwa pembeni ya kiwanda hicho ambapo pia palikuwa na bandari ya mahazi yaliyokuwa yakileta bidhaa kutoka sehemu za Somalia, Arabuni, na India.

"Kazi gani mtu anaweza kupata hapa?" taratibu Rashidi alimwuliza mtu mmoja aliyekuwa amesimama karibu naye pembezoni mwa ukongo wa bahari.

"Nenda kanyonye huko, kazi gani utafanya mtoto kama wewe? Ondoka hapa usije ukapigwa kumbo ukatumbukia baharini."

Rashidi hakutaka tena kuendelea kumwuliza yule mtu, aliendelea na safari yake kidogo kidogo akielekea kule kwenye gati ya majahazi.

Alitamani walau kumwona mtu yeyote yule aliyemjua ili asalimiane naye lakini kila aliyekuwa akimtazama miongoni mwa watu aliokuwa akipishana nao alikuwa ameghadhibika, uso ameukunja. Hakuna aliyemsalimu mwenzake, watu walipigana vikumbo bilaya yeyote kumjali mwenzake.

Moja kwa moja Rashidi aliteremka kwenye gati ya majahazi na alishangazwa na alioyaona huko.

"Lo! nani wale ?" Rashidi alimwuliza kijana mmoja aliyekuwa akichanja kuni, mkono mmoja amekamata shoka na mkono wa pili amejishika kiuno.

"Wako wapi?" aliuliza yule kijana.

"Wale watu waliojipaka rangi nyeusi," alisema Rashidi.

Yule kijana alitabasamu huku akipangusa jasho kutoka kwenye kipaji chake cha uso.

"Hawakupaka rangi wale," alisema yule kijana, "wale, wale wanapakuwa makaa ya mawe kutoka kwenye hayo matishari unayoyaona kule chini," aliendelea.

Rashidi alifurahi sana kupata mtu aliyemwuliza akamjibu. Hiyo ilikuwa ni fursa kubwa kwake kwani tokea alipoanza safari yake kutoka pale penye mlango wa chuma, kila aliyemwuliza alimpuuza na wengine kumtukana bure.

"Makaa ya nani yale?" Rashidi aliuliza, kapigwa na mshangao, kwani watu aliowaona walikuwa wanashughulika kweli.

Wengine walikuwa chini kabisa ndani ya tishari wakizoa makaa kwa maparuo na kuyatia ndani ya vikapu, wengine walikuwa wamebeba vikapu vilivyojaa makaa kwenda kuyamimina kwenye chungu kubwa la makaa lililokuwa kiasi cha yadi hamsini kutoka kwenye yale matishari.

Wachukuzi hao wote walikuwa matumbo wazi wamejifunga shuka fupi viunoni, wenginewalivaa suruali vipande zilizochanika na miili yao ilikuwa myeusi sana kwa vumbi la makaa ya mawe waliyokuwa wakiyabeba.

"Hata sijui makaa ya nani yale, mie naona makaa tu hapa yanateremshwa kila siku," alijibu yule kijana.

"Kila siku ?" huku akiwa ametumbua macho kwa kushangaa Rashidi aliuliza tena, "basi mtu anaweza kupata kazi pale?"

Rashidi alimsogelea kariu zaidi yule kijana akitumainia kupata jawabu la kutia moyo.

"Unaweza ukijaribu, kikapu senti kumi," aljibu yule kijana, "lakini kazi ngumu ile utaiweza weye rafiki yangu ?"

"Nani anayetoa kazi pale? N'tamwendea sasa hivi," kwa hamu Rashidi aliuliza, kwani sas aliona atapata kazi na hatakosa japo shilingi mbili.

"Mwulize yule mzee wa Kishihiri aliyevaa kanzu, koti la kaki na kilemba; yeye ndiye n'nayemwona akishughulika shughulika na wafanyakazi wa pale."

"Kwani weye rafiki yangu jina lako nani?"

"Mie! mie naitwa Saburi."

"Unafanya kazi hapa hapa?"

"Miye ni uledi katika jahazi lile," Saburi alielekea upande wa pili na kuikabili bahari huku akionyesha kidole chake cha shahada upande wa kwenye gati iliyojaa majahazi namna kwa namna akijaribu kumwonyesha Rashidi jahazi lao.

"Jahazi gani?" Rashidi aliuliza kwa shauku.

"Jahazi lile lenye kipaa cha makuti," Saburi aliacha lile shoka alilokuwa nalo mkononi na kuvuta Rashidi mkono ili amwonyeshe jabazi lao kwa uzuri zaidi.

"Ahsante, rafiki yangu, nikipata nafasi n'takuja kutembea jahazini kwenu," Rashidi alimwambia Saburi huku akiendelea mbele kwa hatua ndogo ndogo.

"Lo! usije katika wiki hii mana'ake leo usiku tutatweka kuelekea Pemba na hatutorudi mpaka wiki ijayo."

"Basi rafiki yangu nitakuja kutembea siku yoyote ile," Rashidi alimuaga Saburi na kuelekea kule alipokuwa yule Mshihiri.

Rashidi alimnyemelea yule Mshihiri kidogo kidogo huku akimwangalia kutoka kichwani mpaka miguuni.

Yule Mshihiri alikuwa na furushi la mabati mkononi na mabati bayo yalikuwa yamekatwa duara mfano wa shilingi na alikuwa akiyagawa mabati hayo miongoni mwa wale watu waliokuwa wakibeba vikapu vya makaa ya mawe.

"Washa maskhara yako weye, lazma kigapu nayaza tele," Mshihiri alimwambia mmoja wa wale wachukuzi ambaye kikapu chake hakikijazwa kama inavyotakiwa.

Mshihiri yule alikuwa mkali, jeuri na safihi. Alikuwa akitukana matusi mabaya mabaya akiwa anafanya masihara na kweli humo humo. Wachukuzi walio majabari walimjibu na yeye akazidi kuwatukana kila walipomjibu.

Rashidi alizidi kumsoelea huyu Mshihiri lakini kila alipotaka kumwambia neno alifanya hofu kwa kuchelea kutukanwa. Mwisho alijipa moyo akasema, "Eti Bwana…"

Yule Mshihiri alimtazama kijeuri na mara akamwambia, "ya shekh, nini naataka haba, haba abana bahala ya mshezo."

Yule Mshihiri alikuwa akisema huku uso ameukunja. Kichwa kilikuwa kimezongwa kitambaa cheupe, uso umezungukwa na sharafa ya ndevu nyeusi na nyeupi ambazo kwa juu ziliungana na masharubu yake.

Rashidi hakuthubutu kuendelea na swali lake bali alinyamaza kimya huku akiwaangalia watu waliokuwa wameshuguulika na kazi yao. Alibabaisha kwa kuranda huku na huku na alifika mpaka kule mwisho wa gati ya majahazi ambako walikuwepo watu wakivua samaki kwa mishipi, na baadaye alirejea pale pale aliposimama yule Mshihiri.

"Eti Bwana mie naweza kupata kazi hapa!" Kwa hofu Rashidi alimwuliza tena yule Mshihiri.

"Weye nataka kazi? Naweza kubeba kigabu ya makaa weye?" Yule Mshihiri aliuliza huku akimbinyabinya mikono Rashidi.

"Naweza ! n'tajaribu!" Rashidi alijibu kwa sauti ya juu akiona ameshaitia kazi mkononi.

"Weye bado ndongo! Lenda zake yumbani! Weye habana soma skuli?"

Ijapokuwa umbile la Rashidi lilionyesha nguvu, sura yake ya kitoto ilimdharaulisha.

"Sikiliza mzee," Rashidi alianza "mie naweza kubeba vikapu viwili vya makaa wacha kikapu kimoja," akaendelea bila kujali kitu.

Alikuwa amechoka, taaban. Hamaki ambazo zilisababishwa na kuchoka kwa yule Mshihiri zingelimwezesha kufanya kitu cho chote wakati ule, lakini kila alipofikiri na kuwaza kwamba yeye ndiye aliyekuwa mhitaji ilimbidi astahamili na kuvumilia.

"Sikiliza mzee wangu, mie nisingelikuja hapa kufuta kazi isipokuwa nimeshajiamini kwamba naweza kufanya kazi," Rashidi aliyasema haya kwa udhati wake na hata yule Mshihiri akabaini kwamba Rashidi hakudhamiria kufanya masihara.

"Sikiliza mtoto, ile watu nataka kazi nakuja haba alfajiri sio saa tano, haya enda lenda zako yumbani."

"Sasa kesho nikija alfajiri nitapata kazi sio?" Rashidi aliuliza.

"Lenda! Lenda! Washa kushughulisha mie.

"Wee kalb wee! Weye nashkua kibati mara mbill kwa kikabu moya," mara yule Mshihiri aliyakatiza mazungumzo yake na Rashidi na kumgeukia mfanyakazi mmoja aliyekwi-sha mwaga kikapu cha makaa kwenye ile chungu na sasa alikwenda kuchukua kibati ambacho kilionyesha idadi ya vikapu aliyobeba siku ile. Kila baada ya kumwaga kikapu kimoja mchukuzi alipewa kibati.

Yule mchukuzi aliyekwenda kuchukua kibati alimwambia huyu Mshihiri, "Sikiliza Brek, weye ushazowea dasturi hii, mtu huleta kikapu cha makaa na anapokuja kuchukua kibati unamwambia amekuja mara mbili." Wakati huu kikapu chake kitupu alikuwa amekikamata mkononi.

Kazi ilikuwa imekolea na kila mchukuzi alikuwa atokwa na jasho. Jua la mchana lilikuwa linaunguza na mabanda makubwa ya mabati yaliyoizunguka bandari ya Unguja yalizidisha joto katika eneo hilo.

Mchirizi ya jasho lililokuwa likiwatoka wafanyakazi iliweza kuonekana wazi wazi kwenyp miili yao iliyoharibika kwa vumbi la makaa waliyokuwa wakiyabeba. Kila mtu alikuwa mbioni ana haraka ya kutaka kubeba vikapu vingi ili apate malipo zaidi. Hakuna aliyekuwa na wakati wa kuzung-umza na mwenzake na alielegea kidogo tu alishitukia amesha-tukaniwa mama yake, mkewe au atukanwe yeye mwenyewe tusi baya kabisa.

Rashidi hakutaka tena kuzungumza na Brek, alitulia kimya akisikiliza ugomvi na matusi kati ya wafanyakazi na msimamizi wao. Alisimama hapo kwa muda na mwishowe aliondoka kidogo kidogo akielekea mwisho wa gati ya majahazi waliko wale watu waliokuwa wakivua kwa mishipi. Wote walikuwa wamekaa juu ya ukuta wa bandari na yeye alikaa hapo na kupumua kwa nguvu kwa machofu aliyokuwa nayo.

"Njaa ilikuwa imemshika, asubuhi alikuwa amekula maandazi mawili na kikombe cha chai hapo mkahawani Mlandege. Sasa ilikuwa saa stia na nusu mchana. Pirika pirika nyingi zilimaliza kila kitu tumboni mwake.

Nyumbani kwao mambo hayakuwa mazuri kwani ijapokuwa mama yake alijishughulisha kufanya biashara ya kuuza mbaazi na mboga ya kisamvu wakati wa asubuhi, faida ya biashara hiyo haikumtosha Bi Mashavu kwa mahitaji yake ya kila siku yeye na mwanawe.

Nyumba yenyewe ilikuwa banda tu lililokandikwa dongo na kuezekwa makuti. Hata dari ilikuwa haina. Wakati wa maisika ilivuja kama mwembe, maji ya mvua ykatiririka katika mabati yaliyochomekezwa na kuvijaza vyungu vyote vilivyokuwa ndani. Upande mmoja ulikuwa umevunjika na matundu ambayo yangalimwesha mpita njia kuona ndani wazi wazi yalizibwa kwa magunia makongwe yaliong'ang'anaa kwa moshi wa kuni uliotokea jikoni. Nyumba hiyo haikuwa na chochote ambacho kingelimfanya mtu apende kukaa humo kupumzisha nafsi yake.

Rashidi hakupenda kurejea nyumbani wakati ule na alistahabu kuitisha siku ile hivi hivi akizubaa majiani. Alikuwa na habika kwamba hata akirudi huko nyumbani, atamkuta paka amelala jikoni.

Aliinuka kwa ghafla pale alipokuwa amekaa kama mtu aliyejiwa na fikira mpya. Aliongoza njia ya kule alikotokea mwanzo lakini mara hii alifuata njia ya mkato na kupita katikati ya chungu mbili za makaa ya mawe. Baada ya kwenda kitambo kidogo alimkuta mtu anashughulika kukoroga kitu ndani ya sufuria kubwa. Moto mkali ulikuwa unawaka chini ya sufuria kubwa. Moto mkali ulikuwa unawaka chini ya sufuria hiyo na ilikuwa ni dhahiri kwamba mtu yule alikuwa akipika lakini Rashidi hakuweza kuelewa kitu kilichokuwa kikipikwa.

Rashidi alimsogelea yule mtu karibu na mara yule mtu alimwuliza, "Unataka nini hapa?"

"Sitaki kitu Bwana," Rashidi alijibu.

"Hutaki kitu: tena basi unatafuta nini hapa?"

"Sitafuti kitu mie natembea tu," Rashidi alijibu.

"Weye huna kazi ya kufanya hata unatembea saa hizi?"

"Sina," alijibu Rashidi.

"Huna! Basi njoo hapa mie n'takupa kazi ya kufanya."

Rashidi alifurahi na kwa haraka alimsogolea zaidi yule mtu.

"Kazi! Kazi ya kufanya! Tayari, iko wapi? Nipe nitaifanya sasa hivi," Rashidi alisema huku akitabasamu; kile kitu ambacho akikitafuta kwa muda mrefu sasa amekwisha. kukipata.

"Unaona sinia zile," yule mtu alianza kusema huku akionyesha kidole chake kwenye mnara wa sinia zilizokuwepo chini ya mfereji uliokuwa umekamatana na ukuta wa kijumba kidogo na ambao ulikuwa ukimwagika maji, "Kosha sinia hizo, tena uzikoshe vizuri."

Kwa haraka Rashidi alikwenda mpaka zilipo zile sinia chini ya mfereji na mara alianza kazi ya kuzisafisha.

Zilikuwa nyingi, kiasi ya hamsini hivi, na zilikuwa zimeganda chakula ambacho kilionyesba kimeliwa siku moja au mbili zilizopita.

"Hapana kumbi hapa karibu?" Rashidi aliuliza.

"Kumbi la nini? Sugua hivyo hivyo kwa maji na mchanga," alisema yule mtu.

Rashidi aliifanya ile kazi kwa hima, mara moja moja akimtazama yule aliyemwajiri ambaye alikuwa akishughulika kukoroga chakula alichokuwa akikipika. Baada ya muda kidogo yule mpishi alimaliza kazi yake na mara alimgeukia Rashidi.

"Je! Bado hujesha?"

"N'tamaliza sasa hivi Bwana," Rashidi alijibu.

"Fanya haraka maana saa za kuta zimeshafika, alisema yule mpishi.

"Sasa hivi n'tamaliza, bado kidogo tu," alisema Rashidi.

Kwa haraka Rashidi alikosha zile sinia na alihakikisha kwamba amezikosha sinia hizo vizuri.

"Tayari Bwana," Rashidi alisema akitarajia kazi aliyoifanya itamfurahisha yule mpishi.

Yule mpishi hata hakutazama kama zile sinia zilikoshwa vizuri au hazikukoshwa vizuri.

"Haya zipange hapo chini," alimwambia Rashidi.

Rashidi aliziinua zile sinia na kuanza kuzipanga juu ya kibaraza kilichokuwa hapo chini ya jiko.

Yule mpishi alimwita Rashidi ili amsaidie kuliinua lile sufuria kutoka jikoni, akamwambia "Kamata vizuri, ukilegea litakuunguza".

Rashidi alikamata lile sufuria upande mmoja kwa mikono yake yote miwili na yule mpishi akakamata upande mwingine wakaliinua kutoka pale juu ya jiko.

Baada ya kuliepua lile sufuria, yule mpishi alianza kupakua ugali wa mahindi aliokuwa akiupika, na kuzijaza sinia ambazo Rashidi alikuwa amezipanga juu ya kile kibaraza, moja baada ya nyingine.

"Hizo sinia zilizojaa ziweke upande, unisogezee hizo nyingine."

Rahsidi alifanya kama alivyoambiwa na mara kazi ya kupakua ilimalizika na sinia zote zikawa zimejaa ugali wa mahindi.

Yule mpishi alikwenda uande wa pili wa lile jiko na mara alirejea na kigari kidogo cha mkono. Alikwenda tena mara ya pili kule nyuma ya jiko na aliporejea alikuja na madoo mawili yaliyoonyesha yamjaa, akiwa ameyachukua huku na huku.

"Sasa unajua kijna," mpishi alimwambia Rashidi, "tutazipanga hizi siniz ndani ya hiki kigari na weye utanisaidia hizo ndoo tutakwenda kugawa xhakula huko gatini."

Hapo hapo Rashidi alifanya kama alivyoambiwa. Walizipakia zile sinia za ugali ndani ya kile kigari na baada ya kumaliza waliongozana, yeye na yule mpishi, mpishi akiwa mbele akiburura kigari cha mkono kilicho jaa sinia za ugali na Rashidi yuko nyuma amebeba yale madoo mawili yaliyo-jaa kunde za kuchemsha.

Walifuatana kutoka hapo jikoni mpaka kwenye lile lango la chuma lililokuwa limevamiwa na watu asubuhi. Safari hii lango hilo lilikua wazi na wakapita moja kwa moja mpaka ndani gatini.

Walipofika huko waliwakuta makuli washajipanga wanangojea chakula. Walikaa katika makundi ya watu wanne wanne wakizungumza kwa kelele kubwa.

"Sikiliza weye, ikiwa huwezi kazi basi bora wacha, sisi tumekaa hapa saa nzima sasa tunakusubiti weye utuletee chakula," mmoja kati ya wale makuli alimpigia kelele yule mpishi.

"Wacha kunipigia kelele mie, nenda kampigie kelele mkeo nyumbani," alijibu yule mpishi.

"Mke wangu si weye unayenipikia chakula ukaniletea hapa," yule kuli alisema.

Yule mpishi hakusema kitu tena, alinyamaza kimya huku anaendelea na kazi yake ya kupanga sinia na baadaye kumi-mina kunde juu ya kila sinia aliyoiweka chini.

Matusi ndiyo yaliyokuwa masihara ya huko bandarini. Kila mfanyakazi wa hapo tokea mkubwa wa kazi mpaka yule mtu wa chini kabisa alikuwa ni bingwa wa kutukana kuliko mwenzake.

Makelele yalihanikiza pote hapo. Makuli walikula kwa haraka na baada ya kumaliza walitawanyika kila mtu akaenda kazini pake.

"Kijana! hebu..." yule mpishi hakumaliza alilotaka kusema na alisita kidogo.

"Jina lako unaitwa nani vile?" aliuliza yule mpishi.

"Rashidi, Rashidi Majaliwa."-

"Sikiliza Rashidi, zikusanye hizi sinia zote na halafu uzitie ndani ya kile kigari."

Rashidi aliifanya kazi hiyo na baada ya kumaliza walire-jea kule kule walikotoka.

Walipofika kule jikoni Rashidi alikaa chini na mara yule mpishi aliondoka na baadaye kurejea huku amechukua sinia y ugali mkono mmoja na mkono wa pili alikuwa amechukua kisufuria kidogo kilichojaa kunde.

"Halo, njoo tule na sisi," yule mpishi alimwita Rashidi.

Rashidi ambaye njaa ilikuwa imshika kikweli aliruka pale alipokuwa amekaa na mara alifika ilipo ile sinia ya ugali na kupiga goti. Alikula kikomo ca uwezo wake hata ilimbidi afungue vifungo vya suruali aliyokuwa amvaa ili apate kujishindiia chakula zaidi.

Baada ya kumaliza tu Rashidi hakujiweza tena na alitaftufa penye kivui na kujinyosha. Bila ya kudhamiria usingizi ulimchukua, akalala kama mtu aliyekufa. Chakula alichokula kilikuwa ndiyo mshahara wa kazi ya siku ile ya kuwaandikia makuli chakula huko gatini.

Mzee Shauri, yul mpishi, alimaliza kazi zake zilizobakia baada ya kula na bila ya kumwangalia Rashidi alishika njia akaenda zake.